DAR ES SALAAM: Mwimbaji maarufu wa Marekani, Trey Songz, anatarajiwa kuwasili Tanzania kesho, Agosti 12, 2026 kutumbuiza katika tamasha la IMBEJU Sauti Moja, litakalofanyika Agosti 14 Viwanja vya TTCL, Kijitonyama, Dar es Salaam. Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Foundation, Tully Esther Mwambapa, amesema Trey Songz ndiye msanii mkubwa wa kimataifa anayetarajiwa kutumbuiza katika tamasha hilo. “Tutakuwa na wasanii wengi ambao watatumbuiza katika tamasha hilo, japo msanii mkubwa ni Trey Songz kutoka Marekani. Ujio wake unatarajiwa kuongeza msisimko kwa mashabiki wa muziki nchini, hasa wale wanaofuatilia muziki wa R&B na wasanii wakubwa wa kimataifa. Tamasha hilo litakuwa moja ya matukio makubwa ya burudani jijini Dar es Salaam wikiendi hiyo, likitarajiwa kuwakutanisha mashabiki wa muziki pamoja na wasanii wa ndani na nje ya Tanzania.